Connect with us

News

VIDEO: Hivi Mkenya ana tatizo gani hasa?

Published

on

Na Douglas Mūtūa

MKENYA ni kiumbe jeuri ajabu! Ukimnyima kitu atasonya, akutusi au akwambie hata hakifai kitu. Ni sungura aliyeshindwa kufikia zabibu mtini akasema ‘hata hazijaiva’.

Sasa amekuja juu kwa kuwa amepewa mtihani wa Kiingereza akachimba, sikwambii na visingizio haishi. Uingereza inahitaji wauguzi, lakini si yeyote tu. Kuna viwango vya ubora.

Ikiwa unataka kwenda Uingereza, na sharti ni kwamba uwe na ufasaha wa Kiingereza, ukifeli mtihani usiwe mbuyu ambao ukikosa kuzaa husingizia jua.

Mwanzo unaonekana kama juha unapoanza kuuliza iwapo madaktari walioletwa nchini kutoka Cuba walipita mtihani wa Kiswahili.

Unafaa kuelewa kuwa Cuba si Uingereza, hivyo swali lako hilo libane ubongoni hadi Kenya itakapohitajika kuwapeleka wataalamu Cuba tuone masharti yatakuwa yepi.

Hakuna himaya ambayo haina masharti. Nasikia sharti kuu kwa watakaokwenda jehanamu ni kwamba asitoke mtu nje ya ziwa la moto. Kanuni ya kuungua eti, hali si raha.

Hata hivyo, kwa kuwa haki ni nuru inayotuangazia sote, lazima niseme kuwa ningependa kujua ni mtihani wa aina gani huo uliofanywa na watu 300 wakapita 10 pekee.

Huenda pana jambo; mchakato mzima wa usaili unapaswa kupigwa darubini. Maswali kadha yanaibuka.

Je, mtihani ulikuwa wa kuandika, kusoma au kuzungumza? Mada ya maswali yenyewe ilikuwa afya, sarufi au kitu gani?

Nimesalitika kuuliza maswali haya kwa kuwa picha zilizoibuka mtandaoni zikidaiwa kuwa za mtihani wenyewe zilionyesha maswali ya sarufi. Mtaalamu wa afya… na sarufi? Kioja!

Sarufi ya lugha yoyote ile si kitu cha kukimbiliwa, hivyo kuwapa mtihani wa aina hiyo watu ambao kwa muda mrefu wakipiga miguu jijini kutafuta kazi ni kuwadhulumu.

Ingeeleweka ungekuwa usaili wa kazi ya kufundisha au kuandika ambapo ni lazima watatumia Kiingereza cha kiwango fulani kazini. Wazungu wenyewe hawajui sarufi yao!

Kazi ya uuguzi ilihitaji mtihani wa kuzungumza na kusoma tu – si kuandika – ili uelewa wao wa mambo ya taaluma yao na uwezo wa kuwasiliana uwekwe kwenye mizani.

Huo, nakuhakikishia, visichana vyetu vingepita kwa wepesi wa kupigiwa mfano kwani havinyamaziki vikitema umombo jijini. Hadi utakapovipa kalamu vikuandikie visemayo!

Aliyewapa watoto wa watu mtihani wa Kiingereza wakanoa vilivyo aliwadhulumu kweli ikiwa haukuhusu taaluma yao, lakini hatuwezi kulialia daima kama vitoto.

Mabaya yakikutendekea unayatumia kujifunza na kujirekebisha, au unakata tamaa kabisa na kukwama ulipo.

Hebu tujichungue kama Wakenya; ni kitu gani nchini kwetu kinachofanyika ipasavyo – kwa wakati na katika kiwango kitakiwacho? Huna jibu la moja kwa moja kwa kuwa hakipo!

Tumetelekeza ubora, tukapenda njia za mkato, tukazidi kwa uzembe, matokeo yakawa kuiharibu nchi hivi kwamba fedheha za kimataifa zikitua kwetu haziwi za kushtukiza.

Nipe mfano wa kijana yeyote anayevipenda vitabu, mla jasho lake na shujaa wa uadilifu. Mmoja tu. Labda nikupe muda utafute. Na pengine utamkosa kabisa.

Kisa na maana? Ushirika wa waovu umezuka; mzazi, mwizi, mwalimu na mwanafunzi wanaiba mtihani. Na wakishindwa wanachoma shule moto!

Nia? Mtoto aende chuo kikuu kwa vyovyote vile kwa kuwa thamani ya shahada imepiku akili bora, uwezo wa kufanya kazi na ustaarabu. Ndiyo maana vyuo vikuu uchwara vipo kwenye karibu kila jengo jijini.

Zamani ilikuwa kawaida kwa watu kuajabia: “Anafanya hivyo na ana digrii?” Shahada ziliogopwa na kuheshimiwa.

Leo utasikia watu wakidharau, “Mwache huyo nd’o zake hizo; ana digrii ya kununua!” Dharau, lakini stahiki hasa. Labda hao wa kununua ndio waliotahiniwa na Waingereza?

Sharti tuwe na mwamko mpya wa kusisitiza na kuzingatia umuhimu wa ubora, lau sivyo tutaendelea kuwalaumu wanaotunyima kazi kwa kuwa hatuwezi hata kujiajiri.

MWISHO

Advertisement
Click to comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *