Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliwachekesha wabunge nchini Kenya kwa kusema kuwa wanyama wa Tanzania huingia Kenya, kupata mimba na kurejea Tanzania kujifungua.
Samia ambaye alikuwa kwenye ziara ya siku mbili nchini Kenya, alikuwa kaikihutubia kikao cha pamoja cha mabunge ya Seneti na kitaifa, kwenye majengo ya bunge mjini Nairobi.
Awali, rais huyo aliwataka wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya kushirikiana na si kushindana ili kuhakikisha uchumi wa mataifa hayo mawili unakua huku akitumia lugha ya utani, “Tanzania kuna Suluhu na Kenya kuna Uhuru.”
Alieleza hayo hayo katika kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya linalofanyika Nairobi nchini Kenya ambapo pia lilihudhuriwa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Samia alisema kuingia kwenye ushindani usio na tija hauwezi kuwa na matokeo chanya katika mataifa hayo mawili na kutaka ushirikiano kuwa kitu cha mbele zaidi.
“Mna bahati kwamba nchi zetu mbili upande mmoja kuna Uhuru wa kufanya biashara na upande mwingine kuna Suluhu ya kuondoa vikwazo vya kuendesha biashara kwa hiyo sasa mshindwe nyinyi,” alisema huku akitabasamu na kuwafanya washiriki wa kongamano hilo kucheka.
“Tanzania ipo tayari kuwapokea wafanyabiashara kutokana Tanzania, milango yetu ipo wazi na mikono yetu iko tayari kuwakumbatia. Serikali yangu ipo tayari kuwa daraja katika kuhakikisha biashara na uwekezaji baina ya nchi hizi unafanikiwa.”
Kabla ya Suluhu kuzungumza, Rais Kenyata alieleza kuwa ana matumaini makubwa kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia.
“Sina shaka awamu yetu ya uongozi wa Tanzania, tutaona uhusiano wetu kama majirani na mataifa ndugu ukipanda juu zaidi. Tutatembea bega kwa bega kuhakikisha safari hii tumeitimiza na kuinua uchumi na maisha ya watu katika nchi zetu mbili,” alisema.